Tovuti ya Wikileaks, maarufu kwa kutetea sera za uwazi, imeanza kuchapisha mawasiliano ya siri kati ya balozi za Marekani kuhusu viongozi wakuu duniani.
Baadhi ya mawasiliano yaliochapishwa ni yale kati ya Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia na Marekani, pale alipopendekeza vikali kuwa Iran ishambuliwe kijeshi.Serikali ya Marekani imekashifu hatua hiyo ya kuchapisha mawasiliano hayo. Imesema kuwa kitendo hicho kinahatarisha maisha na mabalozi wake.
Lakini mwanzilishi wa tovuti ya Wikileaks Jullian Assange, anasema serikali ya Marekani haitaki kuwajibishwa.
Wikileaks imechapisha nakala mia mbili kati ya zaidi ya laki mbili ilizonazo ya mawasiliano hayo. Hata hivyo nyaraka zote hizo zimesambazwa kwa magazeti kama vile New York Times la Marekani na The Guardian la Uingereza.
Masuala yalioangaziwa zaidi kwenye mawasiliano hayo ni mpango wa nuklia wa Iran, ufisadi katika serikali ya Afghanistan na uhusiano kati ya serikali ya Urusi na genge la mafia.
Amri ya waziri wa mambo ya nje wa marekani Hilary Clinton kuwa vigogo wa Umoja wa Mataifa akiwemo katibu mkuu achunguzwe pia imechapishwa.
No comments:
Post a Comment