Muda mfupi kabla ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC kutaja majina, na pia kuwaita mahakamani washukiwa wakuu wa ghasia za uchaguzi nchini Kenya , kiongozi wa mashtaka Luis Moreno Ocampo ametoa masharti kadhaa ambayo anataka washukiwa hao wazingatie.
Mapema mwezi huu Bwana Ocampo alifanya ziara nchini Kenya ambapo alikutana na Rais Mwai Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga ambapo serikali ya Kenya ilitoa hakikisho kwamba washukiwa watakaotajwa watatiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani The Hague.
Miongoni mwa masharti hayo ni kuwataka wasiwasiliane wenyewe kwa wenyewe, isipokuwa kupitia mawakili wao wanapoandaa taarifa za utetezi.
Anataka wawe wakiipasha mahakama ya ICC mara kwa mara kuhusu popote walipo, na pia kuhusu namna ya kuwasiliana nao.
Wanatakiwa wasijaribu kuingilia kati ushahidi unaotolewa na mashahidi; Wasiingilie ushahidi uliopo, au kutatiza shughuli za uchunguzi.
Pia wanatakiwa wasijuhisishe na uhalifu mwingine wa aina yoyote.
Zaidi ya hayo wametakiwa kuitikia maagizo yote yatakayotolewa na majaji wa ICC na kwamba lazima wahudhurie vikao vyote vya mahakama wanapotakiwa , na kulipa dhamana wanapohitajika kufanya hivyo.
Ameonya pia kwamba ataitisha kukamatwa mara moja kwa washukiwa ikiwa itadhihirika wanatoa rushwa au kuwashurutisha mashahidi.
Jumatano saa sita kwa saa za Uholanzi Bwana Ocampo anatarajiwa kutangaza majina ya washukiwa hao sita kwenye mahakama hiyo ya ICC.
Mwezi uliopita, aliyekuwa waziri wa elimu ya juu William Ruto alijipeleka mwenyewe The Hague akitaka kukutana na Ocampo, lakini haikuwezekana.
Watu wapatao 1,300 waliuwawa kwenye ghasia zilizofuatia uchaguzi wa Kenya wa mwaka 2007, kufuatia utata kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.
Chini ya usuluhishi wa aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan, makubaliano yalifanyika ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kati ya Rais Mwai Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga.
No comments:
Post a Comment