Mwanzilishi wa tovuti ya Wikileaks, Julian Assange, ambaye uchapishaji wake wa stakabadhi za kidiplomasia za siri umeikasirisha Washington, anajiandaa kuzungumza na maafisa wa polisi wa Uingereza baada ya kupokelewa waraka wa kukamatwa kwake kutoka kwa serikali ya Sweden.
Bwana Assange, anayeaminika kuwa mafichoni nchini Uingereza anatafutwa na serikali ya Sweden ili kuhojiwa kuhusiana na madai ya ubakaji ambayo ameyakanusha.Hapo jana Jumatatu, Uswizi ilifunga akaunti za benki za bwana Assange.
Wikileaks kadhalika imeamua kubadilisha anwani ya wavuti wake mara kadhaa baada ya kuvurugwa mfululizo.
Mkuu wa sheria nchini Marekani, Eric Holder, amezungumza bayana kwamba maafisa wake wanakagua vitabu vya kisheria ili kutafuta njia za kumshtaki bwana Assange kutokana na ufichuzi huo.
Washington imeishutumu Wikileaks kwa kutoa orodha ya maeneo yanayoweza kushambuliwa, kwa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda-baada ya kufichua taarifa kuhusu asasi ambazo Marekani inazingatia kuwa muhimu kwa usalama wake wa kitaifa.
No comments:
Post a Comment