Friday, December 17, 2010

WikiLeaks yamponda rais Bashir

Rais wa Sudan Omar Al Bashir
Stakabadhi za siri za ubalozi wa marekani kuchapishwa hivi punde katika tovuti ya kufichua siri ya WikiLeaks zimedai kuwa rais wa Sudan, Omar al Bashir, huenda aliiba dola bilioni tisa kutoka nchini mwake na kuzificha katika benki ya Lloyds Banking Group jijini London Uingereza.
Katika stakabadhi hiyo, afisa mmoja wa serikali ya marekani anasema kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu, Luis Moreno-Ocampo, alijadili uwezekano wa pesa hizo zilizokuwa katika noti ya dola za marekani kufichwa jijini London baada ya kutolewa kwa waranti ya kimataifa ya kukamatwa kwa rais Bashir.
Afisa huyo alisema bwana Ocampo alikuwa amependekeza kuwa ikiwa mahali pesa hizo ziliwekwa patafichuliwa hatua hiyo itabadili mtizamo wa raia wa Sudan kumhusu rais Bashir.
Msemaji wa serikali ya Sudan alipuuzilia mbali madai hayo na Benki ya Lloyds imesema haina ushahidi unaoonyesha kuwa inahifadhi pesa kwenye akaunti ya jina la bwana Bashir na kwamba daima imekuwa ikiheshimu mfumo wa sheria katika maeneo inakoendehsa biashara.
Mapigano Darfur
Na nchini Sudan kwenyewe wanajeshi wa kulinda amani wa umoja wa mataifa wamesema kumekuwa na mapigano katika jimbo la Darfur kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa kundi la Sudanese Liberation Movement.
Ni mara ya tatu mapigano hayo yametokea wiki hii katika eneo hilo.
Mapigano yameleta mahangaiko kwa wengi Darfur
Msemaji wa umoja wa mataifa Kemal Saiki amesema mapigano hayo yaliyotokea katika kijiji cha Khor Abeche yalikuwa ni makali zaidi.
Zaidi ya watu alfu kumi na mbili wameachwa bila makao katika eneo hilo kutokana na mapigano hayo Wengine wamekuwa wakitafuta hifadhi katika kambi ya wanajeshi wa umoja wa mataifa ambako waliojeruhiwa wanapokea matibabu.
Tangu mwaka 2003, zaidi ya watu alfu mia tatu wameuwawa huko Darfur na takriban milioni tatu wamekimbia makaazi yao.

No comments:

Post a Comment